YANGA MAHAKAMANI KUIFUNGULIA KESI TFF


Kiongozi wa matawi ya Yanga Kaisi Edwin amesisitiza juu ya suala la kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya uchaguzi wao kusimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF, kwa upande wao ni ‘kuisigina’ katiba ya Yanga. “Tutafungua kesi mbili, kesi ya kwanza ni kuomba tafsiri ya kisheria watutafsirie katiba yetu inasemaje na katiba ya TFFinasemaje ili wanayanga tufate nini.” “Kesi ya pili tutamshtaki Rais wa TFF na Katibu wake kwa sababu kwa mujibu wa katiba yao, chombo cha mwisho chenye mamlaka ukiacha mkutano kuu wa TFF ni kamati ya utendaji ya TFF.” “Baada ya sisi kukaa kimya kamati ya utendaji ya TFF ndio watu wa kwanza kuutangazia umma kwa mujibu wa katiba yao na kamati yao ya utendaji walimtambua Yusuf Manji ndio mwenyekiti wa Yanga.” “Lakini kwa makusudi au baadhi ya watu kutaka kuupotosha umma wa watanzania haohao TFF ndio watu wa kwanza kuwaambia wanayanga waende kwenye uchaguzi wa kuziba nafasi ya mwenyekiti wa Yanga.” “Sasa hili mkiliangalia kwa jicho la karibu mtaona ni kosa dogo lakini ni kosa kubwa sana kwa mujibu wa katiba yao. Tutawafikisha mahakamani kwa sababu wameshindwa kuishauri serikali kwa sababu wao ndio walikwenda kuongea na BMT.” “Sisi ushahidi tunao wa barua, watu wa kwanza kupelekewa barua ni kamati ya utendaji ya TFF na hapa ndipo inaibuka hoja ya msingi, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF alipata wapi nguvu ya kimamla kwa mujibu wa kamati yao kum-disqualify mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji kwamba si mwenyekiti na kuitangaza hiyo nafasi kuelekea uchaguzi kama si kutuchanganya sisi wanayanga? “Kwa hiyo tutakwenda ili iwe fundisho kwa viongozi wengine watakaokuja TFF ili waziheshimu taasisi ambazo wanasema ni wanachama wao.”

Post a Comment

0 Comments