IJUE HISTORIA NA MAFANIKIO YA AS VITAL WAPINZANI WA SIMBA LEO HUKO DR CONGO


AS Vita ni timu iliyopo kwenye viunga vya jiji la Kinshasa nchini DR Congo na imeanzishwa mwaka 1935 ikiwa inaitwa Renaissance lakini baadaye mwaka 1939 ikabadilishwa jina na kuitwa Victoria Club. Mnamo mwaka 1971 timu hiyo ikabadilishwa tena jina na sasa ikaitwa Association Sportive Vita Club kwa kifupi AS Vita. Jina la utani la AS Vita ni ‘The Black Dolphins’ au kwa Kiswahili Pomboo Weusi. AS Vita wanapocheza michezo yao mikubwa ya kimashindano hutumia uwanja wa nchi ya DR Congo kwa ajili ya mashabiki wao wengi Stade des Martyrs wenye uwezo wa kubeba watu 80,000. Katika nchi ya DR Congo AS Vita ni timu yenye mafanikio sana katika ligi ya soka nchini humo maarufu kama Linafoot ikiwa imeshinda jumla ya vikombe 14 vya ligi kuu. Vita wapo nyuma ya TP Mazembe ambao wanaaongoza kwa kuchukua vikombe 16 vya ligi ya DR Congo.
Klabu ya AS Vita inashiriki michuano ya kimataifa ngazi ya klabu kama ligi ya mabingwa Afrika maarufu Caf Champions League. Vita imeshiriki katika misimu 14 na kutwaa ubingwa mwaka 1973 wakiwafunga Asante Kotoko ya Ghana huku wakishika nafasi ya pili mwaka 1981 baada ya kufungwa mchezo wa fainali na klabu ya JE Tizi-Ouzou ya Algeria ambayo kwa sasa inafahamika kama JS Kabylie. Mwaka 1978 waliishia hatua ya nusu fainali na kutolewa na klabu ya Hafia FC nchini Guinea kwa goli la ugenini baada ya kufunga magoli 2-0 nchini Guinea na wao kufungwa magoli 3-1 wakiwa nyumbani. Vita hawakuishia hapo kwani mwaka 2014 walicheza pia fainali ya ligi ya mabingwa Afrika na kufungwa na klabu ya ES Setif ya Algeria kwa goli la ugenini baada ya sare 1-1 nchini Algeria na sare ya 2-2 nchini Congo. Katika michuano ya kombe la shirikisho AS Vita imeshiriki michuano hiyo mara nne ikiwa ni pamoja na kufika hatua ya makundi mwaka 2008, 2009 na 2010 huku wakifika fainali ya michuano hiyo mwaka 2018 na kupoteza mbele ya klabu ya Raja Casablanca ya nchini Morocco.
Kikosi chao kitakachocheza leo, kitamkosa beki wake Dharles Mondia Kalonji wa kati baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu kayika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly na Vita kupoteza kwa magoli 2-0. AS Vita ni klabu iliyobarikiwa kuwa na na wachezaji wazuri katika maeneo yote ndani ya uwanja. Miongoni mwa wachezaji wakuchungwa na klabu ya Simba kwenye mchezo wa leo ni pamoja na Ngoma, Moloko Kisinda, Makusu na wengine. AS Vita ina wachezaji watatu tu wa kigeni ambao ni pamoja na golikipa Lukong (Cameroon), kiungo mshambuliaji Omary Sidibe (Mali) na mshambuliaji Aluku (Cameroon) Mara nyingi kocha wa AS Vita Florence Ibenge ni muumini wa soka la kasi na kushambulia haswa anapokuwa nyumbani na ndio maana matokeo yao mengi wanapata kwenye uwanja wao wa nyumbani na si viwanja vya ugenini.
Tangu June 2017 hadi sasa Vita imecheza jumla ya michezo 11 ya ligi ya mabingwa Afrika na ile ya kombe la shirikisho na haijawahi kufungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani. Kila la heri Simba ‘Mnyama’ katika mchezo wa leo mbele ya AS Vita, hakika watanzania wengi wapo nyuma yenu mpate matokeo.

Post a Comment

0 Comments