SportPesa Cup 2019 inaenda Kenya, Tanzania inafeli kwa mara ya tatuKwa mara ya pili mfululizo timu za Tanzania zinashindwa kufanya vizuri katika mashindano ya SportPesa Cup kwenye ardhi ya nyumbani, timu za Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikitegemewa kuleta ushindani katika michuano hiyo na kutwaa taji hilo mbele ya timu za Kenya zimeendelea kunyanyaswa zikicheza nyumbani na ugenini.


Baada ya Simba SC kutolewa kwa kufungwa kwa magoli 2-1 na Bandari ya Kenya, wengi waliweka matumaini kwa timu ya Mbao FC ambayo ilikuwa inacheza nusu fainali ya pili dhidi ya Kariobangi Sharks kutoka Kenya ndio itacheza fainali lakini mambo pia yakawa tofauti na kujikuta wakipoteza mchezo kwa penati 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika wakitoka sare tasa ya 0-0.


Kwa maana hiyo fainali ya michuano hiyo itachezwa kati ya Kariobangi Sharks dhidi ya Bandari zote za Kenya siku ya Jumapili ya January 27 zikitanguliwa na mchezo wa mshindi wa tatu kati ya Simba SC dhidi ya Mbao FC, kwa maana hiyo timu za Tanzania hazijawahi kutwaa taji hilo toka lianzishwe kwake miaka mitatu iliyopita wakati mafanikio makubwa ya timu za Tanzania katika michuano hiyo ni kucheza fainali mwaka jana kwa club ya Simba SC ambayo ilipoteza dhidi ya Gor Mahia.

Post a Comment

0 Comments