Wafuasi wa CHADEMA walipuka kortini, wamuita Mbowe Mandela (+video)


Leo March 6, 2019 Hatimaye Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kutoa hukumu kuhusu dhamana ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kesho Machi 7, 2019.

Mbowe na Matiko walikata rufaa mahakamani hapo baada ya kufutiwa dhamana zao November 23, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Jaji Sam Rumanyika baada ya kusikiliza hoja za warufani na wajibu rufani kupitia mawakili wao.

Jaji Rumanyika amesema amesikiliza hoja za pande zote mbili, hivyo atatoa hukumu Machi 7, 2019.

Awali katika hoja za wajibu rufani kupitia Wakili Peter Kibatala alidai kuwa uamuzi wa kufutiwa dhamana Mbowe na Matiko ulifanyika wakati wote wapo mahakamani.
Amedai kuwa ilikuwa ni makosa kwa Mahakama ya Kisutu kufuta dhamana wakati walikuwepo mahakamani.

Kibatala ameeleza kuwa mazingira hayo waliyofutiwa dhamana washtakiwa haikuwa sahihi kwani ilipaswa kuangalia nini cha kufanya kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Katika hoja nyingine iliyowasilishwa na Wakili Jeremiah Ntobesya ameiomba mahakama itengue uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuhusu kuwafutia dhamana Mbowe na Matiko.
Hata hivyo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi alipinga hoja hizo ambapo amedai hazina msingi wala hazina nguvu ya kuishawishi Mahakama Kuu kutengua dhamana ya washtakiwa hao. 

Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi ya msingi iliyopo Kisutu ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

Video hapa chini ni wafuasi wa CHADEMA waliojitokeza nje ya Mahakama kusikiliza rufani hiyo