ONCE UPON A TIME IN MANCHESTER.
ONCE UPON A TIME IN MANCHESTER.

Muda wa hadithi wajukuu zangu, Ajuni nisogezee kigoda changu halafu mkae kimya niwape simulizi moja ya kale iliyotokea huko Magharibi ya dunia.

Kwanza Maua nimiminie kahawa, halafu Asifa ingia ndani uwaambie wazime redio. Nataka utulivu niwasimulie juu ya Pori moja hatari sana kuwahi kutokea duniani miaka ya nyuma.

Zamani sana huko kwa malkia, huko mjini Manchester Lilikuwepo pori moja la kutisha sana, lilitanda kiza na binadamu waliogopa sana kufika huko. Licha ya kuogopa kwenda huko, maisha yaliwalazimu kwenda na kila mara waliishia kujeruhiwa na kuondoka na maumivu makali.

Hiyo si hadithi ya leo, hadithi ya leo ni juu ya Simba watatu waliokuwepo kwenye pori hilo. Walikuwa wanatisha sana.

Simba wa kwanza alikuwa mwenye njaa sana, alikesha usiku na kushinda mchana akijifunza kuwinda tu. Wenzake hawakumuelewa sana, ila lengo lake alitaka siku moja awe Simba mwindaji bora duniani.

Jitihada zake zilimfanya awafunike wenzake kila ilipofika siku ya kuwinda, uwezo wake uliwashtua wenzake. Hawakuamini kama huyu ni yule mwenzao wanaefanya nae mazoezi kila siku. Alifanikiwa sana hadi kuwa Simba muwindaji bora wa dunia mara tano.

Simba wa pili yeye alikuwa mnyama kweli, labda kwasababu ya asili yake na mitaa iliyomlea. Alitokea katika mapori ya kimaskini huko Argentina. Alijulikana kwa matumizi makubwa ya nguvu katika mawindo yake. Wala hakudumu sana, labda kwa sababu ya ukorofi wake.
.
Simba wa tatu hakutokea mbali sana. Huyu alikuwa mzaliwa wa palepale. Alikuwa na kiu sana ya kuwinda. Alilifia pori lake haswa. Tofauti na wengine hakuwahi kutamani kuondoka kwenda pengine kutafuta mafanikio zaidi. Mpaka kesho anashikilia rekodi ya kufanya mawindo makubwa zaidi ya Simba wote kuwahi kutokea kwenye lile pori🙌.
.
Nakuona Maua unamnong'oneza Mwidini, bila shaka unamuuliza wapo wapi hao Simba sasa na hilo pori lina hali gani?? Si ndiyo??
.
Wale Simba waliondoka, yule mwenye njaa alienda Hispania na sasa yupo Italy, yule muargentina alihamia pori la jirani na baadae kuondoka zake. Yule mzalendo aliishi pale hadi uwezo wake ulipoisha na yeye akaondoka.
.
Lile pori bado lipo lakini Simba waliopo sasa hawatishi kama wale.
.
✍ #salushinetz

Post a Comment

0 Comments