Yanga yatua kwa kiungo MzimbabweKAMA unadhani mabosi wa Yanga wameridhika na majembe iliyonayo kikosi kwa sasa, basi pole yako, kwani tayari macho yao yamenasa kwenye miguu ya kiungo fundi kutoka Zimbabwe anayekipiga Al Hilal waliokuwa washiriki michuano ya Simba Super Cup iliyomalizika jana.

Kiungo aliyeshtua nyoyo za mabosi wa Jangwani ni Last Jesi mwenye umri wa miaka 25 ambaye aliuwasha mwingi kwenye mechi zao mbili dhidi ya Simba na ile ya Tp Mazembe na timu yake ya Al Hilal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mwanaspoti lilinasa mchongo mzima kwa kuelezwa mara baada ya mechi hiyo ya mwisho kwa Al Hilal, huku Jesi akionyesha kiwango cha juu mabosi wa Yanga waliamua kumfuata hotelini akikofikia na timu hiyo na kuzungumza naye.

“Al Hilal walifikia hoteli moja iliyopo Mikocheni na mabosi wa Yanga walishindwa kuvumulia na kumfuata ili kuzungumza na kiungo huyo mwenye mkataba wa miaka mitatu kwa Wasudan.”

Watu hao wa Yanga kuna kiongozi na mabosi wenye ushawishi ambao mara baada ya kumaliza mazungumzo hayo katika hoteli hiyo waliyokuwa wakiweka kambi zamani walimpatia jezi ya timu yao kama zawadi.

Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kwa usiri mkubwa ndani ya hoteli hiyo yalikuwa yanalenga ni namna gani Jesi anaweza kupatikana katika usajili wa dirisha kubwa litakalofunguliwa katikati ya mwaka huu.


Wakala wa mchezaji huyo, George Deda alikiri kufanya mazungumzo na mmoja wa viongozi wa Simba akisema anatamani kumuona Mzimbabwe huyo akija kucheza soka Tanzania.

“Kama itatokea timu yenye uwezo wa kuelewana na Hilal natamani Jesi naye aje kucheza hapa na katika michuano ya Simba Super Cup, amecheza vizuri mechi ya kwanza na Simba aliyoingia kipindi cha pili kama alivyofanya katika mechi na TP Mazembe alichaguliwa kuwa mchezaji bora,” alisema.

Deda ndio wakala wa wachezaji wanne waliokuwa hapa nchini ambao wanatokea Zimbabwe ambao ni, Perfect Chikwende wa Simba na Bruce Kangwa, Never Tigere na Prince Dube wote wa Azam Fc.

Katika hatua nyingine Uongozi wa Yanga, upo katika hatua za mwisho kuboresha benchi lao la ufundi katika eneo la matibabu kwa kumalizana na Daktari wa Ihefu, Nahumu Muganda.

Mwanaspoti lilipenyezewa habari za ndani kutoka Ihefu ambazo zilieleza kuwa Muganda hakuwa na maelewano mazuri kutokana na kudai baadhi ya stahiki zake lakini hata dili hilo la kwenda Yanga lilitokana na ukaribu wa matajiri wa timu hizo mbili.

Katibu wa Ihefu, Athuman Mndolwa alisema daktari wao hayupo katika kikosi chao na alishawaaga akisema anaenda kutafuta changamoto mpya timu nyingine kubwa iliyokuwa katika Ligi Kuu Bara.

“Baadaye tukaja kufahamu kuwa kuna kiongozi mkubwa kutoka GSM aliwasiliana na mmoja wa mabosi wetu hapo ndio ikatoka ruhusa ya Muganda kwenda kuanza kazi katika kikosi hicho cha Yanga,” alisema.

“Baada ya kutuaga tupo katika mchangamoto wa kutafuta daktari wa timu mpya mwenye uwezo kama wake ili kuendelea kuwapatia tiba stahiki wachezaji katika kikosi chetu,” alisema Mndolwa

Post a Comment

0 Comments